Contact   |   Site map  


 

 
 

Client Service Charter

MKATABA WA HUDUMA KWA WATEJA

(CLIENTS SERVICE CHARTER - English Version to be uploaded soon)

Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM -TAMISEMI) ni kiungo muhimu kati ya Wizara za Kisekta na Asasi mbalimbali za Serikali za Mitaa.Ofisi hii inalo jukumu la kuhakikisha kuwa yanajengwa mazingira mazuri ya kuwezesha ushirikishwaji wa Umma katika kujiletea maendeleo yao wenyewe. Mambo muhimu yatakayozingatiwa ni Utawala Bora na kuboresha utoaji huduma ngazi za Serikali za Mitaa. Aidha jukumu letu ni kuwahudumia wateja wa ndani na nje.

Chini ya mpango uliopo wa Uboreshaji wa Huduma kwa Umma, OWM - TAMISEMI, inategemewa kuongoza na kuwa kiungo kati ya Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa na Mpango wa Uboreshaji wa Wizara za Kisekta unaofanywa na Sekta mbali mbali ngazi ya Taifa. Katika kutekeleza jukumu hili la kisera, OWM - TAMISEMI, ina majukumu ya kiutendaji yafuatayo:-

1. Kuratibu na kusimamia Tawala za Mikoa ili ziweze kuzisaidia Halmashauri katika kutekeleza wajibu na majukumu yake;
2. Kutayarisha na kusimamia Sera ya Maendeleo Vijijini;
3. Kusimamia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Mijini;
4. Kuendeleza Programu ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa nchini ili ziweze kutoa huduma bora;
5. Kuzijengea Serikali za Mitaa uwezo wa kusimamia mapato na matumizi;
6. Kuboresha miundo, hali ya watumishi na mifumo ya kazi ndani ya OWM - TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri;
7. Kusimamia Asasi, Mashirika ya Umma na Miradi inayotekelezwa chini ya OWM - TAMISEMI;
8. Kuratibu utekelezaji wa shughuli za hifadhi ya mazingira katika Serikali za Mitaa;
9. Kuratibu vita dhidi ya rushwa na UKIMWI.

Katika kuyatekeleza majukumu hayo, OWM - TAMISEMI inafuata misingi ya uwazi na uwajibikaji kwa umma kwa shughuli zote za Serikali, kiasi kwamba mfumo wa ukaguzi wa mara kwa mara, tathmini na kusambaza matokeo umeandaliwa kikamilifu. Taarifa kuhusu huduma zilivyotolewa itatayarishwa na kutumwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kila mwaka. Hii itasaidia umma kujua mafanikio na matatizo ya utekelezaji wa malengo ambayo OWM - TAMISEMI ilijipangia kwenye Mkataba wa Huduma kwa Wateja. Madhumuni ya Mkataba huu wa Huduma kwa Wateja ni kuongeza ufahamu, ubora na upatikanaji wa huduma zitolewazo na OWM - TAMISEMI. Mkataba huu utawawezesha Wateja kuelewa majukumu ya OWM - TAMISEMI na namna ya kufanya mawasiliano nao endapo viwango vya huduma ni duni, na namna ya kushugulikia malalamiko ya Wateja inapotokea kwamba huduma zilizotolewa hazikuridhisha. Wateja pia watakuwa na uwezo wa kupata haki zao kwa malalamiko yatakayothibitika kuwa ni ya kweli. Ieleweke pia kwamba Wateja wana wajibu wa kuzingatia kikamilifu na kufuata kanuni za maadili na tabia njema zitakazojenga mazingira mazuri ya utoaji huduma.

Kwa madhumuni ya kudumisha mahusiano bora na Wateja, tunashauri Wateja wetu kuleta malalamiko yanayoihusu Ofisi hii kwanza kabla ya kuyapeleka katika vyombo vingine vya nje. Ukosoaji wenye nia ya kujenga pamoja na kutoa mrejesho kuhusu huduma zinazotolewa na Ofisi hii unakaribishwa kama vile zinavyokaribishwa pongezi na maoni kuhusu namna ya kuboresha huduma zinazotolewa.