Contact   |   Site map  


 

 
 

SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA LATIMIZA MIAKA 40 TANGU KUANZISHWA KWAKE

Date: 16th Jan 10
8:00am - 6:00pm
Location: Kibaha
Contact Person: IEC UNIT
Contact Telephone:
Attached Document:



Shirika la Elimu Kibaha, KEC tarehe 16 mwezi huu litaadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Kanali Mstaafu Ferdinand Swai alisema kuwa maandalizi ya maadhimisho hayo yanaendelea vizuri. Shirika la Elimu Kibaha  lipo umbali wa kilomita 48 kutoka Dar es Salaam, katika barabara kuu iendayo Morogoro.

Ni miongoni mwa mashirika machache ya umma, yaliyofanikiwa kuonyesha matunda yake, tofauti na mashirika mengi yaliyoanzishwa miaka ya 1970, ambayo sasa yamekufa au kubinafsishwa, baada ya kushindwa kujiendesha.

Hivi sasa KEC lipo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) na linamiliki shule ya msingi Tumbi na sekondari ya kutwa ya Tumbi.

Pia, shirika hilo linamiliki sekondari ya Kibaha ya bweni (wavulana), sekondari ya Kibaha ya bweni (wasichana), Chuo cha Maofisa Tabibu cha Tumbi, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha, Hospitali ya Tumbi na mashamba ya kilimo na mifugo.

Ni dhahiri kwamba uwajibikaji na mikakati mizuri inaliwezesha shirika hilo kusonga mbele, likiwa na uwezo wa kukabiliana na ushindani mkali, ulioletwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia na mfumo wa utandawazi.

Uwezo wa shirika hilo unatia moyo, kwamba litaendelea kuwa urithi wa vizazi vijavyo, ikiwa ni pamoja na kutunza kumbukumbu za historia ya mambo mazuri, yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Shirika hilo lilianzishwa mwaka 1963 kwa ushirikiano wa nchi za Denmark, Sweden, Finland na Norway, wakati huo likiitwa Nordic Tanganyika Project (NTP).

Lengo la kuanzisha mradi huo lilikuwa kuwapatia Watanzania elimu bora ili waweze kupambana na vita dhidi ya ujinga, maradhi na umasikini na kujihakikishia maisha bora na endelevu.

Ingawa nchi hizo za Nordic zilitoa mchango mkubwa, Serikali ya Tanzania ilishiriki bega kwa bega katika harakati hizo za kuhakikisha wananchi wanakuwa na maisha bora na endelevu.

Baada ya kuendesha mradi huo kwa miaka saba, nchi za Nordic ziliamua kuukabidhi kwa Serikali ya Tanzania kwa Mwalimu Nyerere Januari 10, 1970.

Kitendo hicho kilisababisha mradi huo kubadilishwa jina na kuwa Shirika la Elimu Kibaha.

Shirika la Elimu Kibaha linafanya kazi zake kwa sheria ya Bunge namba 17 ya mwaka 1969 ya uundaji wa mashirika ya Umma. 
 


 
  January 2010  
S M T W T F S
          1 2
3 4 5 6 7 8 9
10 11 12 13 14 15 16
17 18 19 20 21 22 23
24 25 26 27 28 29 30
31            

<< back to list of events.