Wananchi wa Vijiji vinavyouzunguuka Msitu wa Ngong’olo katika kata ya Mikese Mkoani Morogoro wametakiwa kujiendeleza katika suala la ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kujiongezea kipato.
Mratibu wa Mpango Shirikishi wa Hifadhi ya Misitu(PFM) bwana Francis sekibaha alisema hayo hivi karibuni wakati alipoutembelea Msitu huo mkoani Morogoro ambapo aliwataka wananchi kuitumia fursa hiyo kujiongezea kipato.
Alisema kuwa licha ya kulinda hifadhi ya Msitu huo wa asili wananchi hawana budi kujishughulisha na ufugaji wa nyuki, na kilimo cha uyoga ambacho mtaalamu huyo alisema ni rafiki wa mazingira na hivyo wananchi wanaweza kuitumia fursa hiyo kujiongezea kipato.
Picha hii huonesha Mradi shirikishi wa Vikundi vya Ufugaji Nyuki katika Msitu Ngong’olo Mkoani Morogoro.
Alisema kuwa ikiwa dhana hii ya usimamizi Misitu shirikishi itaendelezwa itawezesha Misitu kuhifadhiwa vema na wananchi
Msitu wa Ngong’olo licha ya kuwa na eneo zuri la kuhifadhi misitu, ni miongoni mwa Misitu ya asili iliyopo nchini ambayo ina baadhi ya miti kama Mpingo na Mninga ambayo ipo hatarini kutoweka.
Nao wakazi wa vijiji vinavyouzunguka Msitu huo waliiomba Serikali isaidie katika juhudi zao za ulinzi dhidi ya uchungaji holela wa mifugo ambao unatishia kutoweka kwa misitu ya asili nchini.
Salum said mmoja wa vijana wanaolinda msitu wa Ngong’olo alisema kuwa kuwepo kwa jamii ya wafugaji katika eneo hilo ni tishio katika juhudi zao za kuulinda msitu huo wa asili.
Aliongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa sheria ndogo ya kusimamia msitu huo, bado utekelezaji wake umekuwa changamoto kutokana na vipengele vilivyomo katika sheria hiyo kutokubalika katika mahakama kwa kigezo kuwa mahakama zimekuwa zikitumia sheria mama.
Alisema kutokana na kikwazo hicho mara nyingi wahalifu wanapokamatwa na kupelekwa mahakamani wamekuwa wakiishia kupewa faini ndogo ambazo wamekuwa wakizilipa kwa urahisi.
Kutokana na changamoto hiyo, Mratibu wa PFM alizitaka kamati za mazingira za vijiji vinavyouzunguka Msitu huo kuzingatia taratibu walizojiwekea ili ziwawezeshe kusimamia uhifadhi wa mazingira wa Msitu huo.
Posted: 4th Mar 10 by IEC UNIT
|