Contact   |   Site map  


 

 
 

WAZIRI MKUCHIKA AAGIZA MIKOA YOTE ISHIRIKI UMITASHUMTA MWAKA UJAO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Kapteni Mstaafu George Mkuchika ameagiza kuwa katika mashindano ya mwaka ujao mikoa yote itapaswa kuleta timu zao ili zishiriki katika mashindano ya UMITASHUMTA.


Pichani kulia, Mheshimiwa Waziri wa Nchi OWM-TAMISEMI Kapteni Mstaafu George Mkuchika pamoja na Waziri wa Elimu Dokta Shukuru Kawambwa wakisalimia na wachezaji wa timu ya Mkoa wa Singida ambayo ilipambana na timu ya Mkoa wa Morogoro na kufungwa magoli matatu kwa bila.


Waziri Mkuchika alisema kutokana na umuhimu wa sekta hiyo kuendelezwa mashuleni ameagiza uongozi wa mikoa yote nchini kuhakikisha kuwa inaleta timu zao kushiriki katika mashindano hayo ili kuibua zaidi vipaji vya watoto.


Alisema michezo hiyo ni muhimu sana kwa vijana katika kuibua na kuendeleza vipaji vyao na akadai kuwa michezo ni nyenzo muhimu na rahisi ya kuitangaza nchi katika medani za kimataifa.


Alikumbushia tukio la mwaka 1974 ambapo mwanariadha wa kimataifa kutoka Tanzania Filbert Bayi aliposhinda mbio za dunia, vyombo vya kimataifa viliweza  kumtangaza sana mwanariadha huyo na hivyo kuiweka juu ramani ya Tanzania duniani.


Mheshimiwa Mkuchika akataka Taifa lijipange ili kuweza kurejesha heshima ya Tanzania kimataifa kama alivyofanya Filbert Bayi kwani Serikali ipo bega kwa bega na wadau wa michezo katika kuhakikisha kuwa sekta hiyo inakua nchini na inatumika vilivyo kulitangaza Taifa na vivutio vyake mbalimbali.


Mbali na hilo, Waziri Mkuchika aliziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuhakikisha kuwa zinatenga bajeti inayostahili katika Idara na vitengo vya utamaduni katika mamlaka hizo.


Alisisitiza kuwa kufanya hivyo kutasaidia mamlaka hizo kuwaendeleza wanamichezo katika mamlaka zao, tofauti na sasa ambapo alikiri kuwa kiwango cha fedha kinachotengwa hakitoshi kutimiza majukumu hayo.


Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mheshimiwa Dokta Shukuru Kawambwa alisema kuwa Wizara yake itahakikisha kuwa inashirikiana na OWM_TAMISEMI katika kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana ili waweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.


Alisema wizara hizo mbili zitashirikiana kwa pamoja kuhakikisha kuwa shule zote zinazosajiliwa zinakuwa na viwanja vya michezo.

 







Posted: 17th Dec 10 by IEC UNIT
<< back to list of News.