Contact   |   Site map  


 

 
 

WAZIRI MKUU AWATAKA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO YA KIUTAWALA KATIKA MSM

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda (Mb) amewakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya juu ya wajibu wao wa kuzisimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa na kwamba ugatuaji umefanyika tu katika majukumu ya kimaendeleo.


Akizungumza na Viongozi hao tarehe 21 Mei, 2012, wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Siku 10 kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya yanayoendelea mjini Dodoma, Waziri Mkuu alisema Majukumu ya Serikali kwa shughuli za kiutawala hayajagatuliwa kutoka Serikali kuu kwenda Mamlaka za Serikali za Mitaa.


Alifafanua kuwa ugatuaji umefanyika tu katika majukumu ya kimaendeleo ambapo fursa imetolewa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kupanga na kutekeleza kwa uhuru shughuli za maendeleo kwa kuzingatia Sera, Mipango na Mikakati ya Serikali kuu.


Waziri Mkuu aliwataka Viongozi hao kutambua majukumu hayo waliyopewa ili waweze kuwasaidia wananchi kuondokana na umasikini.


Huku akinukuu maneno ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwamba Mhe. Pinda alisema ‘Kiongozi anayetakiwa kwa Taifa letu, lazima awe anakerwa na matatizo ya Wananchi’.


“Ninyi kama  Viongozi na Watendaji Wakuu katika maeneo yenu ni timu muhimu katika kufahamu changamoto, matatizo na kero  walizonazo wananchi hasa wale wanaoishi vijijini ambao ni aslimia 80  ya Watanzania wote katika  kuwasaidia kuondokana na umasikini.” Alisema


Waziri Mkuu aliongeza kuwa kuongoza ni kuonyesha njia ya nini kifanyike ili kukabiliana na changamoto na malalamiko ya wananchi. Aliwataka Viongozi hao kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wananchi baadala ya kuwa sehemu ya matatizo yao.


Aliwaasa kutambua na kukubali kuwa uongozi ni kufanya kazi zaidi na kwa hiyo ni majitoleo kwa umma na siyo nafasi ya kujinufaisha binafsi au ofisi ya kupiga mbwembwe.


“Ni aibu kwa RC au DC kuomba chakula kwani si kweli kwamba hapakuwa na fursa nyingine za kuepuka hali hiyo. Fursa za kuzalisha mazao mbadala zipo, himizeni watu wenu walime mazao yanayostahimili ukame, yanayokomaa kwa muda mfupi na ikibidi muwasisitize wazalishe chakula cha ziada ili wawe na akiba ya kutosha na pia waweze kuuza na kupata fedha.”


Waziri Mkuu alisema kuwa baada ya mafunzo hayo anatarajia kila Mkuu wa Mkoa au Wilaya  kujiuliza kiwango cha umaskini katika eneo alilopangiwa na kuangalia pato la wastani la mwananchi katika wilaya au mkoa wake na kuainisha kama ongezeko la idadi ya watu katika mkoa au wilaya yake linaendana na ukuaji wa uchumi katika eneo husika.

 

“Mnapaswa pia kuzijua na kuzitambua fursa za kiuchumi zilizopo ndani ya mkoa au wilaya husika; mziainishe ni fursa zipi za kiuchumi za haraka zinazoweza kumtoa mwananchi kwenye umaskini na zaidi ya yote myaangalie ni kwa namna gani mwananchi wa kawaida atawezeshwa kutumia fursa zilizopo kuondoa umaskini unaomzunguka.”


Aliwataka kuhakikisha kuwa maeneo yao yanakuwa na miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa viwango stahiki na nidhamu katika ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za umma na kujiridhisha kuwa zinatumika kwa manufaa ya wananchi.


Mafunzo hayo yanashirikisha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa na.


Jumla ya Mada 39 zimepangwa kujadiliwa  ambazo ni pamoja na kazi na majukumu ya mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya, mawasiliano ndani ya wilaya, majukumu ya serikali za mitaa, uhusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, mgawanyo wa madaraka na uhusiano miongoni mwa mihimili mitatu ya Dola.


Nyingine ni maadili ya viongozi na nafasi ya madhehebu ya dini katika kujenga umoja wa kitaifa.

 







Posted: 25th May 12 by GC UNIT
<< back to list of News.